UTANGULIZI KATIKA KITABU CHA "JIFUNZE KUCHANA"


Rap (uchanaji) ni nguzo ambayo imo katika utamaduni wa Hip Hop. Nguzo za Hip Hop kwa mujibu wa Africa Bambataa (cited in Hanzi, 2012) zinatajwa kuwa nguzo za Hip Hop ziko Tano (Machata, Udijei, Uchanaji, Mabreka na Maarifa) lakini kwa mujibu wa UN (2001) kupitia azimio la amani la Hip Hop lililopitishwa na wanaharakati zaidi ya 300 wa Hip Hop na mashirika na taasisi nyinginezo zinaongezea nguzo nne (Ujasiriamali, Mitindo ya Mtaani, Lugha ya mtaani na midundo kinywa). Hali hii inafanya kuwepo kwa makundi mawili yanayoamini kuwa nguzo za Hip Hop ni tano na yanayoamini nguzo za Hip Hop zimeongezeka na kuwa Tisa.
Rap kwa Kiswahili sanifu huelezewa kama ni kitendo cha ku – “sema kwa ghafla au kwa ukali” (Tuki, 2000). Kuna uwezekano mkubwa hii imetokana na uwiano, kwamba maelezo haya yatakuwa yametokana na ile tafsiri ambayo Bahati (2011) anayosema kuwa “Muziki huu ulikuwa unaitwa “muziki wa kufokafoka” kipindi hicho”. KBC (2008) anasema “Neno kufoka foka ni neno la kibaguzi kwa wachanaji kama neno ‘N’ kwa mtu mweusi.. Neno hilo lilianzishwa na waandishi wa habari wa kitanzania wenye uelewa mdogo na wasiojua chochote kuhusu muziki wa Rap na hata walipoelezewa vizuri waligoma kuuita unavyopaswa (Muziki wa Rap) wakaamua kuuita Muziki wa kufoka foka.
Tafsiri sahihi ya Rap inaelezewa na Bahati (2011) anaposema “hilo jina (kufoka foka) halikuwa sahihi, na uliupa mziki huu taswira mbaya. Lakini kwa kuwa ulikuwa ni muziki mpya, inawezekana hatukujua jina gani litakuwa sahihi… Muziki huu ulionekana ukiwa na hiyo dhana ya kufokafoka, na kawaida ya tamaduni zetu, mtoto hamfokei mzazi. Hivyo inawezekana Hip Hop ikaonekana ni muziki unaochochea uasi dhihi ya tamaduni zetu…. neno sahihi la Kiswahili ni kughani” au Michano (kuchana) kwa mujibu wa zavara (2012).
Kwa tafsiri hizo, ni wazi kwamba mtu anayefanya muziki wa Rap au “Rapper” kwa Kiswahili huitwa Mchanaji au Mghanaji. Hivyo katika kitabu hiki nitatumia neno Mchanaji kumaanisha Mghanaji au “Rapper”. Rap na Hip Hop inaonekana kama ni maneno mbadala kwamba neno Rap humaanisha Hip Hop na neno Hip Hop humaanisha Rap. Ukweli ni kwamba “Rap na Hip Hop sio maneno mbadala” (Dubois na Bradley, 2010). Kiuhalisia, Rap ni Moja kati ya nguzo zinazounda Utamaduni wa Hip Hop hivyo Rap ni kijisehemu cha Hip Hop, Zavara (2012) anasema “kipengele cha michano ndicho kinachovuma sana….. na kufanya hata Baadhi ya watu kufikiri kuchana ndio Hip Hop.
Ni ukweli usiopingika kwamba sio kila mwenye uwezo wa kuchana anaweza kuwa ni Mchanaji wa Hip Hop japo Muziki wa Rap hujengwa kwa uchanaji. Kwa kawaida mchanaji wa Hip Hop huitwa “Mc” na mchanaji wa kawaida huitwa “Rapper” na hii ndiyo sababu hata katika aina nyingine za muziki kwa Mfano: dansi kuna marapa.
Stic Man (cited by Zavara, 2012) anasema, “Ni kama vile kuwe na mpiganaji wa mapigano ya kitaa na mtu aliyefunzwa na kufuzu sanaa ya mapigano”. Kawaida mpiganaji wa mtaani ni mpiganaji, lakini huyu aliyefuzu na mfanyaji mazoezi ya sanaa ya mapigano anakuwa na uwezo wa ziada. Huu mfano ndio tofauti kubwa iliyopo kati ya mchanaji wa kawaida na MC (Zavara, 2012).
Mchanaji wa kawaida (Rapper) ni yule mchanaji mwenye uwezo wa kuchana ambaye hana uelewa kuhusu utamaduni au mwenye uelewa kuhusu utamaduni wa Hip Hop lakini hafuati au hachani katika Misingi, kanuni na taratibu za uchanaji katika utamaduni wa Hip Hop lakini Mchanaji wa Hip Hop (Mc) ni yule mchanaji mwenye uwezo wa kuchana kwa kufuata misingi, kanuni na taratibu za uchanaji zilizopo katika utamaduni wa Hip Hop.
Myka 9 (quoted in Edwards, 2009) wa Freestyle Fellowship anasema anasema kuwa “wachanaji wa sasa wamejengwa kutokana na misingi ambayo iliyoachwa ”. Hapa tunaona kwamba kuna neno “Misingi” ambayo inaweza kuwa Misingi ya Uandishi na Misingi ya Hip Hop. Neno “Iliyoachwa” ni wazi limeficha nomino Fulani, ukisikia neno “Iliyoachwa” ni lazima ujiulize maswali mawili. (a) ni ipi iliyoachwa na (b) ni kina waliyoiacha. Swali la kwanza jibu lake itakuwa iliyoachwa ni misingi na waliacha misingi hiyo ni waliotangulia kwa maana ya wakongwe. Hivyo ili ujifunze Misingi ni lazima ujifunze kutoka kwa waliotangulia kama P The Mc (personal communication, 2014) anavyosema “Ukiwa na ndoto ya kuwa Mc ni vema ukawaona watu waliokutangulia, ukawaomba ushauri juu ya kitu gani ufanye ili uweze kuwa mchanaji mzuri”.
Kitabu Hiki kimelenga kuelezea vitu ambavyo ni muhimu mchanaji awe navyo ili aweze kuwa Mchanaji wa Hip Hop kama ambavyo tumekwishaona kwamba kuweza tu kuchana hakumfanyi Mchanaji kuwa mchanaji wa Hip Hop. Kitabu hiki kinahusisha taarifa kutoka katika vitabu, makala, maazimio, dokumentali, wanaharakati, nyimbo za wasanii, mahojiano na mbinu nyinginezo ukusanyaji wa taarifa. Imani yangu ni kwamba msomaji ataweza kujifunza mambo mengi yahusuyo sanaa ya uchanaji katika utamaduni wa Hip Hop.
kimeandikwa na
Malle Marxist
© 2014
KINAPATIKANA
Mawasiliano: 0715076444

0 Comments: