HIP HOP INA NGUZO WABONGO HAMZIWEZI

Wakati Madee alipotoa kibao cha “Hip Hop Haiuzi”. Kila mwanahiphop alikuwa na neno lake aliloweza kulizungumza. Wachanaji wengi wameshamchana katika nyimbo zao tangu kibao kimetoka mpaka leo anaendelea kuchanwa hata wachanaji wanaochipukia. Katika kibao hicho kuna mahali Madee anasema “Hip Hop ina Nguzo, bongo hamziwezi”. Ni kauli nyepesi kuitamka lakini ukitumia mawanda mapana ni ngumu kuifafanua ikaeleweka katika maana mahsusi kutokana uelewa wa Moja moja uliopo .
Katika kujadili kauli hii “Hip Hop ina nguzo, bongo hamziwezi” nitatumia maswali mawili kufafanua kauli hii. Swali la kwanza ni “Je Hip Hop ina nguzo, Nguzo za Hip Hop ni zipi” na la pili “Je ni kweli nguzo hizo za Hip Hop wabongo hawaziwezi?”. Nitatumia maswali hayo kupima usahihi na uhalali wa kauli hiyo.
Swali la kwanza. “Madee alisema kwamba “Hip Hop ina Nguzo”. Ni kweli kabisa alikuwa sahihi kusema hivyo. Katika kitabu changu cha “Chuo Kikuu cha Hip Hop” niliandika kwamba mwanzoni nguzo za Hip Hop zilitajwa na Africa bambataa kuwa ni nne ambazo ni Machata, Mabreka, Uchanaji na Udijei. Nguzo nyingine iitwayo Maarifa iliongezeka na kuzifanya ziwe tano.
Katika azimio la amani la Hip Hop (Hip Hop Declaration of Peace) lililofanyika katika umoja wa mataifa (UN) mwaka 2001 na kusainiwa na wanaharakati na taasisi mbalimbali zaidi ya 300 waliongeza nguzo nne ambazo ni “Ujasiriamali wa mtaani, Mitindo ya mtaani, Midundo kinywa na Lugha ya mtaani” na kuzifanya nguzo za Hip Hop kuwa Tisa.
Hata hivyo bado kuna mgongano wa hoja kutokana na kuwepo kwa pande mbili ambzo zinaamini nguzo za hip hop ni tano na upande mwingine ukiamini nguzo za Hip hop zimeongezeka na kuwa Tisa.
Swali la pili ambalo linauliza “Je ni kweli nguzo hizo za Hip Hop wabongo hawaziwezi?” ni swali ambalo linanifanya nijiulize maswali mengine mengi. Kama ambavyo nimekwisha kuelezea na kuzitaja Nguzo za Hip Hop hapo juu.
Nachojaribu kuelewa, hii ni namna nyingine kusema kwamba “wabongo hatuwezi kuwa wachanaji, wabongo hatuwezi kuwa madijei, wabongo hatuwezi kuwa mabreka, wabongo hatuwezi kuwa wachata, wabongo hatuwezi kuwa na maarifa, wabongo hatuwezi kuwa wajasiriamali, wabongo hatuwezi kupiga Midundo kinywa na wabongo hatuwezi kufanya mitindo ya mtaani.
Nikimuuliza mtu kama Mejah Mbuya kwamba wabongo hatuwezi kuwa wapiga machata nafikiri atanijibu… “Nenda Ubalozi wa Uingereza.. ukawaulize wale wazungu kwanini walikubali ukuta wao tuupige machata..”. ama nikamuulize Dj Bony Luv kwamba “wabongo hatuwezi kuwa madijei” lazima ataniuliza “..kwani wewe umenifahamu vipi..?”
Inawezekana Madee akawa anamkubali Mc mmoja tu Tanzania mpaka sasa kwa maana kuna nyakati (kama sio mwaka jana basi mwaka huu) alishawahi kusema anamkubali sana Nash Mc na ndiye mc wa kweli anayefanya hip hop Tanzania..
Napata shida kupata usahihi wa kauli hii… kwamba “Hip Hop ina Nguzo wabongo hawaziwezi” huenda mchanaji alikuwa na maana yake mahsusi ambayo ni tofauti na hii ambayo nimeielezea hapo juu.. usiangalie Chini…. NIMEANGUSHA CHENCHI….
Imeandikwa na
Malle Marxist
0715076444
©2014

0 Comments: